|
Tanzania
Leo
Undani wa Utamaduni wa Mtanzania Kisiasa
Respicius Shumbusho Damian
Toleo la 1: Tulikotoka
Tazania inajulikana sana katika historia kama “Kisiwa cha Amani,” jina
amabalo lilitumika kufikisha ujumbe kwamba ni nchi ambayo hakuna wala haitegemewi
kuwepo machafuko ya aina yoyote ya machafuko na vurugu za kisiasa, kikabila,
kiitikadi au mambo mengine ambayo yangesababisha vita. Jina hili liliifanya Tanzania kutengwa kimtazamo na chi za Africa karibia zote ambazo nyingi zimepitia historia ya
vita hasa kuanzia miaka ya 1960 Uhuru wa Afrika. Tanzania ikawa sehemu ya kupumzikia
wageni kutoka nchi mbali mbali ambao wengi walikimbia machafuko na ubaguzi wa
rangi katika nchi zao. Mwarabu, mzungu, mswahili, mhindi, mchina, na kadharika
waliweza kuishi nchi moja na kuifurahia amani japo tukikumbuka hadi miaka ya
1980 katika baadhi ya Miji mikubwa mfano Dar es salaam, Mwanza na mingine
ilikuwa ni kitu cha kawaida kutofautisha mitaa kwa kutumia rangi yaani Mtaa
mwingine kuitwa Uswahilini (Kwa watu wa hali ya chini), mingine uzunguni (watu
wa hali ya juu) na mingine Uhindini au Uarabuni (hii ikiwa ni mitaa ya watu wa
hali ya kati wakiwemo waafrika matajiri wa kati).
Uzungu, uhindi, na uswahili haukikua na
kusababisha kutofautiana. Hata hivyo mzazi wa taifa tunayemkumbuka kwa jina la
baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Raisi wa kwanza wa
Tanzania alizidi kuwakuza watoto wake ambao mbali na utofauti wa kipato,
makabila, makazi, rangi na mengine mengi, katika imani ya kwamba wao ni wamoja
na mshikamano,umoja na kupendana ndiyo misingi ya familia kubwa ya mtanzania.
Vile vile hata yule aliyetofautishwa kwa jina la rangi yake mfano mzungu au
mwarabu alibakia kuheshimika na kufurahia amani kati ya matunda mengi ya uhuru.
Miaka ya 1980 ambapo nchi nyingi za Afrika
zilikuwa katika mgawanyiko wa kiitikadi, baadhi zikifuata na kuamini misingi ya
siasa za magharibi (yaani ubepari) zikiongozwa na Marekani, na zile za
mashariki(yaani Ujamaa ambao una chembe nyingi za kikomunisti). Kaman chi
nyingi zilivyofanya kujitangaza kuamini ujamaa kutokana na makovu ya ukoloni, Tanzania ilijitahidi kujenga ujamaa wa kiafrika ambao ulizidi kusisitiza umoja na haki
kwa wote. Katika harakati hii waliokuwa na utajiri mkubwa usiojulikana
ulivyopatikana walikosa amani kwa kiasi Fulani,japo hakuna mtu wa kabila moja
aliyepigana na kumnyang’anya wa kabila lingine mali yake wala wa rangi moja
kufanya hivyo kwa mtu wa rangi nyingine. Neno ‘Umma’lilisaidia kutunza amani.
Kila ambaye mali yake ilitaifishwa alimchukia huyo Umma ambaye ilikuwa ni vigumu kumpata.
Mali nyingi na njia kuu za uzalishaji mali zikawa mali ya umma, ambaye wachambuzi wengi wamemlaani kwani machungu yake juu ya mali hizo yalikuwa ni kidogo sana na hivyo kuwaacha wajanja wachache
kuendelea kujifaidisha huku wengi wakiendelea kuwa maskini. Nje ya yote haya
watanzania waliendelea kuushika usia wa baba Nyerere wa kuilinda amani pamoja
na kwamba ilikuja kugeuka nyundo ya kuwakandamiza wanyonge ambao walikuwa
wanaona kuwa waliopewa mamlaka kusimamia na kulinda mali ya umma kwa niaba ya
wananchi wanajilimbikizia mali wenyewe huku wananchi wakizidi kuteswa na maadui
wakuu watatu wa taifa letu. Kimsingi jitihada zote ikiwemo utaifishaji wa njia
kuu za uzalishaji mali zililenga kupigana na kuulia mbali hawa maadui wakuu watatu, yaani umaskini, maradhi
na ujinga.
Huenda nimlaumu mwalimu aliyefundisha na
kuturithisha tamaduni nyingine za taifa letu (kikiwemo kuheshimu na kunyenyekea
mamlaka, kuvumilia kupita kiasi, kuipa kipaumbele amani kuliko chochote,
kupinga ukabila na pengine woga kwa mwananchi wa kawaida) alishindwa au
alisahau kufundisha utamaduni wa kuiweka haki kileleni mwa yote na kuwarithisha
viranja wake tamaduni kama vile kuheshimu mali ya umma, kutanguliza maslahi ya
taifa kabla ya maslahi binafsi na uchu wa madaraka. Baadhi ya tabia hizi
zimekua na kulifanya taifa letu likiwa na viongozi wa aina tatu; Kwanza wapo
wale ambao wana njaa kama punda, hata wale usiku kucha hawashibi(humu ndimo
ufisadi, rushwa, upendeleo na ufujaji wa mali ya umma wanapatikana). Pili,
wapo ambao wananapenda kila mwananchi aendelee na kuufurahia uhuru na utamu
kisiwa cha amani lakini wanazidiwa nguvu sana na hawa wenzetu ambao mizizi yao
imeenda chini sana kiasi kwamba kuwang’oa ni kazi ngumu.Pia wanaogopa sana hawa
wa kundi la kwanza kwani ni rahisi sana kuhatarisha maisha yao mara tu
wakionekana wanawazibia mirija yao haramu inayowapatia kipato kisicho halali.
Na mwisho wana mtandao mkubwa wa nguvu ya kiuchumi kutoka nje na ndani ya Tanzania, HIVYO
ni vigumu kutikiswa.
Kundi la tatu ni la wachapakazi na wapenda
maendeleo ya wote, lakini bado tu hawawezi kufanikiwa peke yao kwani wanawahitaji sana hawa wa kundi la kwanza ambao pamoja na ubovu wao wote tuliousikia wana siraha
iitwayo uzoefu. Hawa ni kama Waganga wanaotegemewa sana kufanya tambiko siku hadi siku ili
serikali yetu iwepo na nchi yetu izidi kuwa na amani (japo mimi imani hii naona
siyo ya kweli). Muda mwingine viongozi wetu wazuri wanatambua kuwa tunaweza
kuendelea bila kuwa na watu hawa, lakini wanaogopa kuwatia aibu kwani
waliheshimiwa tangia taifa letu lipate uhuru. Kwa maana nyingine; wao ni picha
ya taifa, uchafu walionao ndani yao ukiwekwa wazi kwa umma na watu kutoka nje watagundua kuwa taifa na serikali
yetu ina uchafu uliojificha ndani yake ambao kwa kuwa na macho madogo hawawezi
kuuona.
Hivyo inabidi tutambue kabisa kwamba kuna
mambo makubwa manne (i) Historia yenyewe imetujenga na tukawa tulivyo hivyo
mabadiliko ya historia yenyewe yatazidi kutubadili hadi mwisho wa historia.
(ii) Tofauti ni kitu cha kawaida katika jamii yoyote na ndizo huibua kasi ya
mabadiliko, hivyo hata zikifichwa kwa muda mrefu kwa njia Fulani mwisha
historia yenyewe itaziibua tofauti ili ziweze kuiruhusu historia ya jamii hiyo
kuwepo na kupiga hatua. (iii) Lazima jamii au serikali yoyote iwe na mazuri na
mabaya; japo walio madarakani hupenda yatangazwe mazuri tu, mwisho wa yote
tofauti kati ya viongozi wenye dhamana ya kuiongoza jamii hiyo huzaliwa na
historia, na tofauti hizi hubeba chembe za ukweli, kutokubaliana, uwazi na
misuguano mingi (hata umwagaji damu). Hii ndiyo huishia katika mabadiliko na
kukubaliana kwa muda hadi mabadiliko mengine yajitokeze. (iv) Tofauti na migogoro hailengi kuvuruga amani;
malengo makuu ni kuisahihisha jamii, ila katika masahihisho ya jamii yoyote
migogoro, vurugu, uadui na kusutana ni dalili za kawaida.
Basi tofauti ndivyo zilivyoanza kati ya
watanzania, hasa hasa miaka ya 1990 ikifuatia mabadiliko yaliyokuwepo ulimwengu
mzima. Mabadiliko haya ni pamoja na kukua kwa mawazo ya kimagharibi kama vile Demokrasia, Haki za binadamu, Soko Huria na
siasa vya vyama vingi. Mabadiliko haya Tanzania yamekuja kufuatia ulegevu wa misukumo ya siasa za kijamaa kutoka nchi za Ulaya
mashariki (hasa Urusi) ambao ulikuwa unayapa mlango mawazo ya kimagharibi ambao
kwa wengine wanayatazama kama ukombozi wa
fikra.
Naweza kukubali kuwa upepo wa siasa za
magharibi umeleta mabadiliko makubwa katika siasa za Tanzania ambazo kwa tangia 1977
zilijengewa imani ya msingi kwamba kuwepo chama kimoja kutasaidia katika
kudumisha mshikamano na umoja katika kujenga taifa. Mapema miaka ya 1980
ilikuwa si rahisi kukubalika kuunda mashirika ya kiraia ama vikundi vyovyote
ambavyo vingeikosoa serikali ikidhaniwa kwamba ingechangia kuangusha umoja na
kutoa nafasi kwa kuzaliwa kwa uasi kwa serikali.
Ni kweli kwamba umoja ulikuwepo, lakini
vile vile wajanja wachache walitumia nafasi hiyo kuwanyima haki raia wema
kuikosoa serikali na idara zake maana kila jaribio la kuungana kuikosoa
serikali lilionekana kama uasi au jaribio la
kuleta migawanyiko. Mbali na suala la haki serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kwa
wengi ilionekana kushika kila nafasi ya maamuzi na kuulinda mfumo na imani za
chama badala ya mawazo ya raia. Kwa wengine hadi mwaka 1985 ilikuwa ni vigumu
kutofautisha chama na serikali ikiwa ni pamoja na viongozi wa chama
kuwashurutisha watendaji wa serikali kutenda si kwa utalamu bali kulinda
itikadi na imani ya chama. Ndani ya hali hii miradi yote tuliyoita ya umma hapo
awali ilikufa kutokana na usimamizi mbaya.
Hali hii ilipelekea kuvipa nguvu vikundi
vya kiraia na kuzaliwa utofautiono wa mawazo na mwisho mfumo wa vyama vingi
Tanzania Mwaka 1992. Tangu kuanza kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini
yapata miaka18 iliyopita, bado uwezo wa vyama kusimama kama vyama kwa maana ya kushika hatamu mbalimbali za uongozi ni mdogo.
Kadiri mfumo huo unavyozidi kupata umri ndivyo msisimko wake unavyoonekana
kuzidi kupungua hususani kwa wananchi ambao bila kuvikubali haviwezi kuimarika.
Wanaharakati na wafuasi wanaeleza kuwa sababu ni pamoja na; muundo wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, matumizi mabaya ya vyombo vya dola hususani wakati wa
uchaguzi na mikutano na mihadhara ya kisiasa ambayo ndio hupaswa kutumika
kueneza sera za vyama husika.
Vile vile ikiangaliwa kwa undani kuna ukosefu wa elimu ya uraia miongoni mwa
wananchi ambayo ingewafanya watambue umuhimu wa ushiriki wao katika mambo ya siasa,
upinzani wa wazi na kuondoa hofu ya kutengwa baada ya kujiunga na vyama vya
upinzani. Hivyo vyama vimekuwa vikikosa nguvu tena za kutetea na kusimamia
mambo ya msingi ambayo yamekuwa kero kwa wananchi na badala yake kutoa mwanya
kwa asasi za kiraia na zisizo za kiserikali, kuwa wakosoaji wa serikali, jambo linaonekana
kutoifurahisha serikali siku zilizopita.
Ukweli ni kuwa idadi kubwa ya Watanzania ni
wenye elimu ya chini na ndio wanaoongoza katika kujihusisha na masuala mengi ya
kisiasa kama kujiandikisha kupiga kura, kuhudhuria
mikutano ya siasa pamoja na kushangilia matokeo ya chaguzi. Wanaokubaliana na
mfumo wa vyama vingii ni wale ambao wana elimu ya kutosha katika kuchangia
maoni ya msingi na sera lakini hukosa ushiriki wa moja kwa moja katika kuunga
mkono vyama. Naamini kuwa vyama vina sera nzuri isipokuwa havijajulikani
ipasavyo na kuenea kutokana na ukosefu wa uwezo wa kujikimu kiuchumi. Upo umuhimu
wa wananchi kuelimishwa kuhusiana na elimu ya uraia ili kutambua umuhimu wa
kushiriki katika mambo muhimu ili jukumu libaki kwa wananchi wenyewe kuamua
chama cha kukiunga mkono badala ya kuwafanya wauone upinzani kama uasi au ugaidi. Kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka 2005 nilikuwa katika jimbo la
Karagwe wilayani Karagwe-Mkoa wa Kagera nilichojifunza ni kwamba watu wengi
wamejengewa imani kwamba wafuasi wa vyama vya upinzani hawana akili timamu.
Pamoja na dhana potofu iliyostawi Tanzania kuwa nia ya vyama hivi ni upinzani tu
katika kila jambo, vimekuwa muhimu katika kuwaamsha viongozi usingizini na
kuwahimiza kuongoza kwa haki, uwajibikaji na kuweka maslahi ya wananchi mbele
badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi. Naamini kwamba kufa kwa vyama vingi vya siasi kungepelekea utawala wa
kidikteta wa chama kimoja ambacho ni wazi kuwa kilizoea kutumia ubabe katika
kuamua.
Mpaka sasa tunakubaliana kuwa wabunge wa upinzani humezwa kila wakati
linapokuja suala la maamuzi muhimu bungeni. Hili ni kovu la enzi za mfumo wa
siasa ya chama kimoja ambapo viongozi waliegemea zaidi katika kulinda maslahi
ya chama badala ya maslahi ya wananchi ambao kila kukicha wamekuwa wakiumizwa
na makali ya maisha na umasikini.
|